Jumamosi, 8 Aprili 2017

Bangi kuuzwa katika maduka ya dawa Uruguay

Bangi kuuzwa katika maduka ya dawa Uruguay


Uruguay itaanza kuuza bangi kwenye maduka ya dawa kuanzia Julai.
Nchi hiyo ya Marekani Kusini itakuwa ya kwanza duniani kuuza Bangi kihalali kwa matumizi ya kujiburudisha tu.
Safari ya kuhalalisha matumizi ya bangi ilianza mwaka wa 2013 baada ya sheria iliyokubali uuzaji na ununuzi wake kupitishwa.
Hata hivyo imechukua muda mrefu kwa sheria hiyo kuanza kutumika.
"Bangi itauzwa kwenye maduka ya dawa kuanzia Julai," msaidizi wa Rais, Juan Andre Roballo alisema katika kikao na wanahabari.
Sheria hii inawataka wanunuzi kujisajili na serikali. Bei yake itakuwa $1.30 kwa gramu moja.
Watakaojisajiliwa lazima wawe raia wa Uruguay au wakazi wa kudumu wa nchi hiyo na hawaruhusiwi kununua zaidi ya gramu 40 kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Marijuana hiyo itakuwa inapandwa kwenye mashamba yanayosimamiwa na serikali.

Sheria pia inawaruhusu wanaotumia bangi kupanda mimea yao nyumbani au kujiunga na vikundi vya sacco vinavyokuza mimea ya bangi.
Wauzaji wengi wa dawa hata hivyo wanasema wanashuku iwapo watapata faida yoyote ikiwa tayari bei yake imewekwa.
Baadhi ya wanunuzi pia hawakubaliani na amri ya serikali ya kuwasajili kwanza kabla kuwauzia bangi wakisema ni uvamizi wa hali yao ya faragha.
Vile vile hawakubaliani na pendekezo la kuwapimia kiwango cha bangi wanachonunua .
Tayari serikali imeandikisha mkataba na maduka 16 ya kuuza madawa na inatarajia kusajili maduka zaidi.
Roballo amesema kuwa kutakuwa na kampeni ya afya itakayofanywa kabla ya sajili kufunguliwa rasmi.
Alisema kuwa serikali kwa sasa haina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya wanunuzi lakini haitarajii idadi yao kuwa kubwa zaidi.