Ijumaa, 7 Aprili 2017

Marekani yaishambulia Syria kwa makombora

Mgawanyiko wa hisia kufuatia mashambulio ya Trump dhidi ya Syria


Kombora kutoka kwenye meli za kijeshi za Marekani katika bahari ya Mediterranea
Kumekuwa na shutuma na uungwaji mkono wa makombora iliyofyetuwa Marekani dhidi ya Syria.
Inategemea ni upande upi wa mzozo huo mataifa yanaunga mkono.
Mataifa yanayo unga waasi wanaopambana na utawala wa rais wa Syria Bashar al Assad, yameunga mkono shambulio hilo.

Baadhi ya watoto walioathirika na kemikali,Syria
Uturuki imepokea vizuri ufyetuaji makombora hayo, wakati afisa wa wizara ya mambo ya nje wa Saudia amemsifu rais Trump kwa ukakamavu wake na Uingereza imejitolea usaidizi kikamilifu.
Waziri mkuu wa Israel amesema ujumbe wa wazi umetumwa unaopaswa kusikika sio tu Damascus lakini pia Iran na Korea kaskazini.
Kwa upande wake Iran ambayo kama Urusi inaunga mkono serikali ya Syria imeshutumu shambulio hilo.

Serikali ya Putin anasema kiongozi huyo amepokea kwa utulivu taarifa hiyo
Moscow imetaja mashambulio hayo kama uchukozi mkali dhidi ya taifa huru. Msemaji wa rais Putin (Dmitry Peskov) amesema kwamba kando na kukiuka sheria za kimataifa , Washington imesababisha uharibifu mkubwa katika uhusiano na Moscow.
Wizara ya mambo ya nje imetangaza kusitishwa kwa makubaliano na jeshi la Marekani yalioundwa kuzuia mashambulio ya angani anga ya Syria.
Katika taarifa kwenye televisheni Jeshi la Syria limesema watu 6 wameuawa na mali kadhaa kuharibiwa kutokanana shambulio hilo la makombora