Jumamosi, 8 Aprili 2017

SUA kumkumbuka hayati Sokoine kwa mhadhara.



WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, anatarajia kumwakilisha Rais Dk John Magufuli katika muhadhara wa 14 wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwenye maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 33 ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Kwanza , Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekufa kwa ajali ya gari.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Gerald Monela alisema kuwa maadhimisho hayo yataanza Aprili 10, mwaka huu kwa upandaji wa miti sambamba na shughuli za maonesho ya kazi za tafiti mbalimbali , utoaji wa huduma kwa wakulima na jamii ikiwa na zoezi la upimaji wa afya utakaoendana na michezo.
Alisema mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa ni Waziri wa Kilimo , Mifugo na Uvuvi Dk Tizeba ambaye atamwakilisha Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Aprili 12, mwaka huu siku ya muhadhara huo.
“Muhadhara huu na shughuli zingine zitafanyika katika kampasi ya Solomoni Mahlangu ( Mazimbu) ambapo mada kuu ya kumbukizi ya miaka 33 tangu kifo cha Sokoine ni Matumizi ya Kilimo zana kwa Maendeleo ya nchi kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati,” alisema