Jumapili, 6 Agosti 2017

Arsenal wameibuka mabingwa wa ngao ya hisani kwa mwaka 2017 baada ya kuitundika Chelsea kwa mikwaju ya penati 4-1 kufuatia dakika 90 za kawaida za mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1

.

Mpira ulianza kwa kasi kidogo huku ukichezwa eneo la katikati ya uwanja lakini Arsenal ndio walionekana kuutawala zaidi mpira na kufanya shambulizi la kwanza dakika ya tano  baada ya krosi ya Hector Bellerin kutoka mashabiki mwa lango la Chelsea kuishia mikononi kwa Thibaut Courtois huku pia dakika mbili baadae Alex iwobi akimtoka vyema David Luiz na kupiga pasi ndani ya boksi ambayo ilikosa mmaliziaji.
Arsenal waliendelea kulisakama lango la Chelsea baada ya Danny Welbeck kupiga kichwa kilichodakwa vyema na golikipa Thibaut Courtois kufuati akrosi ya Granit Xhaka kutoka katikati ya uwanja huku dakika mbili baadae Courtois alifanya kazi ya ziada kuokoa mchomo wa Alex Iwobi aliyegongeana vyema na Mohamed Elneny na kuwa kona.
Alexander Lacazette alikaribia kuiandikia Arsenal goli la utangulizi dakika ya 23 ya mchezo baada ya shuti lake kumshinda Thibaut Courtois na kugonga mwamba kabla ya kuokolewa na walinzi wa Chelsea
Per Mertesacker alipata majeruhi dakika ya 28 ambayo yalimlazimu kutoka nje ya uwanja baada ya kugongana na Gary Cahill vichwani na nafasi yake kuchukuliwa na Sead Kolasinac.
Per Mertesacker akigugumia kwa maumivu baada ya kuumia kufuatia kugongana vichwa na Gary Cahill wakati wa purukushani za kuwania mpira. 
Chelsea walianza kutawala kiungo na kuishambulia Arsenal kwa kushtukiza ambapo Petr Cech alikuwa ‘busy’ kuokoa mashuti yaliyopigwa kuelekezwa langoni kwake na Willian pamoja na Pedro ambaye alipokea pasi nzuri ya Willian kutoka mashariki mwa uwanja na kuachia shuti kali lililookolewa kwa ustadi mkubwa na Cech
Mwamuzi Robert Madley alikuwa mkali kama mbogo baada ya kuwaliwa wachezaji kadi za njano mfululizo huku Willian, Pedro pamoja na Azpiliqueta wakiwa wahanga, na hadi mpira unamalizika dakika 45 matokeo yalikuwa 0-0
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo sekunde chache tu, Victor Moses aliindikia chelsea goli la kuongoza baada ya kuwazidi ujanja walinzi wa Arsenal waliodhani ameotea na kuunganisha vyema krosi iliyopigwa na Gary Cahill kwa kichwa
Victor Moses akiifungia Chelsea goli la kuongoza dakika ya 46 ya mchezo
Arsenal walicharuka na kuanza kulisakama lango la Chelsea kama nyuki ambapo Thibaut Courtois alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la mbali la Mohamed Elneny ambalo lilipigwa kwa mfumo wa krosi huku dakika chache baadae akiokoa kombora la umbali wa takribani mita 30 lililopigwa na Granit Xhaka.
Iliwabidi Chelsea wacheze pungufu kufuatia Pedro kupewa kadi nyekundu baada ya kumcheza rafu mbaya kiungo wa Arsenal, Mohamed Elneny
Dakika tatu baadae mlinzi Saed Kolasinac aliandikia Arsenal bao lakusawazisha kwa kichwa akiunganisha krosi mujarabu kutoka kwa Granit Xhaka na baada ya hapo Arsenal walianza kushambulia mfululizo huku Walcott akikosa nafasi mbili za wazi ambazo zote ziliishia mikononi wa Thibaut Courtois.
Sead Kolasinac akishangilia baada ya kuifungia Arsenal bao la kusawazisha dakika ya 83 ya mchezo
Dakika 90 zilikamilika kwa sare ya bao 1-1 ambapo ilifuata changamoto ya mikwaju ya penati.
Cahill alifunga penati ya kwanza kwa upande wa Chelsea kabla ya Theo Walcott na Nacho Monreal kufunga mfululizo. Penati ya Thibaut Courtois pamoja na Alvaro Morata kwa upande wa Chelsea ziliota mbawa na kisha Alex Oxlade-Chamberlain na Olivier Giroud kumaliza kazi na kushinda kwa jumla ya penati 4-1.
Olivier Giroud akishangilia baada ya kupiga penati ya mwisho ya ushindi
VIKOSI:
Chelsea: Thibaut Courtois, Cesar Azpiliqueta, David Luiz, Gary Cahill (C), Victor Moses, Cesc Fabregas, NG’olo Kante, Marcos Alonso/Antonio Rudiger, Willian/Charlie Musonda Jr, Pedro, Michy Batshuayi/ Alvaro Morata
Akiba:
Willy Caballero, Andres Christenses, Antonio Rudiger, Kyle Scott, Jeremie Boga, Charlie Musonda Jr.
Arsenal: Petr Cech, Rob Holding, Per Mertesacker (C)/ Sead Kolasinac, Nacho Monreal, Hector Bellerin, Mohamed Elneny, Granit Xhaka, Alex Oxlade-Chamberlain, Danny Welbeck/Neiss Wilson, Alex Iwobi, Alexandre Lacazette/Olivier Giroud
Akiba:
David Ospina, Sead Kolasinac, Joel Willock, Ainsley Maitland-Niles, Olivier Giroud, Theo Walcott, Reiss Nelson