Madhara 10 ya vidonge vya kupanga uzazi kuzuia mimba
Vidonge vya Uzazi wa Mpango, ni moja ya njia inayopendekezwa na Wataalamu wa Mpango wa Uzazi katika kuzuia mimba. Hata hivyo, vidonge hivyo vinaweza kutimiza malengo hayo ya mpango huo ikiwa tu vitatumiwa vizuri na kwa usahihi, kwa sababu tafiti zilizopo, zinaonyesha kwamba asilimia nane (8%) ya wanawake hupata mimba zisitarajiwa kila mwaka, huku wakiwa katika mpango huo kutokana na baadhi yao kujisahau kumeza vidonge hivyo.
Kwa mujibu wa tafiti hizo ambazoFikraPevu inazo, vidonge hivyo vya mpango wa uzazi vikitumiwa vizuri, kwa kuhakikisha muda wa matumizi yake unakuwa ule ule, ni mwanamke mmoja pekee kati ya 100 anayeweza kupata mimba isiyotarajiwa ndani ya mwaka wa kwanza wa matumizi ya dawa hizo.
Hadi sasa kuna aina kuu mbili tu za vidonge vya uzazi vinavyotumiwa na wanawake katika wa mpango huo, ingawa aina zote hizo zina vichocheo (hormons). Aina hizo kitaalamu zinaitwa Estrogen na Progesteron. Estrogen ni aina ya kichocheo kinachotengenezwa na uterasi/kizazi, kinachosaidia kurekebisha mzunguko wa hedhi, kwa kuongoza ukuaji wa kuta za uterasi kwenye sehemu ya kwanza ya mzunguko wa hedhi.
Kwa upande wake, Progesterone, hiki ni kichocheo cha kopasi luteamu ya ovari, kinachosaidia kuanzisha mabadiliko katika endometriumu baada ya ovulesheni.
Ingawa katika aina hiyo mbili ya vidonge, kuna vingine vina kichocheo cha aina moja tu, kwa maana ya ama Estrogen au Progesterone, huku vingine vikiwa na vichocheo vyote viwili hivyo, lakini vidonge vyote hivyo ni salama, na vinafanya kazi kwa kufanya ute mzito kwenye shingo ya mji wa mimba na kuzuia kupevuka kwa yai, hivyo kuzuia mimba kwa kiwango cha asilimia 99.
Vidonge vya uzazi wa mpango vinaweza pia kutumika kama tiba ya kuweka sawa mzunguko wa hedhi, kuzuia maumivu makali wakati wa hedhi, kutibu chunusi pamoja na kupunguza hatari ya magonjwa katika via vya uzazi, ambayo hayatokani au kusababishwa na magonjwa ya ngono.
Hata hivyo, pamoja na usalama wa vidonge hivyo katika kufanya kazi yake hiyo ya kuzuia mimba na tiba kwa magonjwa hayo, vidogo hivyo vinaweza kumsababishia athari za kiafya mwanamke kama havitumiki katika mpangilio sahihi.
- Athari kuu 10 zinazoweza kusababishwa na vidonge hivyo ni pamoja na kutokwa na damu ukeni baada ya hedhi ya kawaida. Kwa mujibu wa wataalam wa mpango huo, athari hiyo huweza kuwapata asilimia 50 ya wanawake wote wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango. Hali hii huweza kuwatokea ndani ya miezi mitatu baada ya kuanza matumizi ya dawa hizi. Kwa ujumla, hali hiyo huweza kukoma kwa zaidi ya asilimia 90, pindi mwanamke anapoanza kutumia pakti ya tatu ya dawa hizo katika kipindi hicho cha kutokwa damu ukeni. Mwanamke anapotokewa na hali hiyo kwa mfululizo wa siku tano au zaidi baada ya kumaliza siku zake za kawaida za hedhi, anashauriwa kuwasiliana na mhudumu wa afya wakati akiendelea kutumia dawa hizo.
- Athari ya pili, ni kujisikia kichefuchefu. Mara nyingi hali hiihumtokea mwanamke mwanzoni tu baada ya kuanza kumeza vidonge vya uzazi wa mpango, ingawa hali hii inaweza kukoma baada ya siku chache. Inashauriwa pia kwa mwanamke anayepatwa na hali hii ya kichefuchefu kuwasiliana na mhudumu wa afya kama ataona hali hiyo inazidi.
- Matiti kujaa au kuwa na maumivu, ni athari nyingine inayoweza kusababisha na matumizi ya vidonge hivyo. Hali hii huweza kumpata baada ya kuanza kutumia vidonge hivyo, na huweza kukoma ndani ya wiki moja tu. Hata hivyo, inashauriwa kwamba ikiwa matiti hayo yatatokwa na uvimbe au maumivu yasiyoisha, ni muhimu kutafuta tiba kwa wahudumu wa afya, ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya kinywaji chenye kafeini (caffeine) na chumvi na kuvaa brauzi isiyobana matiti.
- Maumivu ya kichwa ni athari nyingine inayoweza kumtokea mwanamke, ingawa pia kuumwa kichwa kunaweza kuwa na dalili za magonjwa mengine. Hata hivyo, kama itatokea maumivu hayo ya kichwa yakaanza tu mara baada ya kumeza vidonge hivyo, hiyo itakuwa ni dalili ya athari mojawapo na ni vyema kutoa taarifa kwa mhudumu wa afya.
- Vidonge vya uzazi wa mpango huweza pia kuongezeka uzito wa mtumiaji, ingawa tafiti nyingine zimeshindwa kuthibitisha uhusiano kati ya vidonge hivyo na mabadiliko ya uzito wa mtumiaji. Aidha, baadhi ya wanawake hupatwa na tatizo la maji kuganda kwenye matiti na maeneo ya nyonga baada ya kutumia vidonge hivyo.
- Mabadiliko ya hisia huweza pia kumtokea mwanamke anayeanza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango. Inashauri kwamba pindi mwanamke anapoona dalili hii, ni muhimu kumjulisha mhudumu wa afya ili kuweza kujadili ni jinsi gani ataweza kutumia dawa hizo, kwa sababu dalili hii ni mbaya kiafya kwa mtu mwenye historia ya ugonjwa wa Kushuka Moyo (Depression).
- Athari nyingine ya dawa hizi ni kutokwa na uchafu ukeni. Baadhi ya wanawake, mara tu baada ya kutumia vidonge hivi hutokwa na uchafu ukeni, ikiwa ni pamoja na kupatwa na uwezekano wa kupungua au kuzidi kwa ute wakati wa tendo la ndoa. Ni muhimu sana mwanamke anapobaini dalili hizi, kuonana na mhudumu wa afya ili kubaini kama hali hiyo imesababishwa na athari ya vidonge au kuna maambukizi ya magonjwa ya zinaa.
- Wanawake wengine huweza kujikuta wakikosa siku zao za hedhi baada ya kutumia vidonge vya uzazi wa mpango. Ingawa ugonjwa wa msongo wa mawazo (stress), magonjwa, mchoko wa safari unaweza kusababisha hali hii, lakini inashauriwa kupima kama mtu amaepatwa na ujauzito hata kama anatumia vidonge hivi kama itatokea kukosa hedha katika mazingira tata.
- Kupungua kwa hamu ya kufanya tendo la ndoa ni athari nyingine inayoweza kumkuta mwanamke anayetumia vidonge vya uzazi wa mpango kutokana na vichocheo vilivyomo ndani ya dawa hizo, ingawa pia magonjwa kama ya kisukari, shinikizo kubwa la damu na kadhalika yanaweza pia kuchangia tatizo hilo.
- Athari ya 10 na ya mwisho kwa wanawake wanaotumia vidonge hivyo, ni mabadiliko ya taswira ya kitu anachokiona mbele yake, hasa kwa wanawake wanaovaa miwani ya macho. Kwa kuwa macho ni moja ya eneo muhimu la ufahamu kwa mwanadamu, hali hii inapowapata wanawake, inashauri kuonana mara moja na daktari wa macho pindi tu dalili hizi zinapoanza kujitokeza.
Ni tahadhari gani mwanamke anatakiwa kuchukua kabla na baada ya kuanza matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango?
Kwa mwanamke mzazi, hairuhusiwi hata kidogo kuanza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango ndani ya wiki tatu tu baada ya kujifungua mtoto au ikiwa atakuwa ananyonyesha mtoto mwenye umri wa chini ya miezi sita.
Aidha, ikiwa mwanamke amefanyiwa upasuaji mkubwa wa aina yoyote katika siku za karibuni, au kama mwanamke husika ni mvutaji wa sigara na ana umri wa zaidi ya miaka 35, haruhusiwi kutumia vidonge hivyo, kama ambavyo pia haruhusiwi kufanya hivyo mwanamke mwenye historia ya ugonjwa wa ini, manjano, moyo, saratani ya matiti, tumbo la uzazi pamoja na shinikizo la damu linalobadilikabadilika kila wakati kwa viwango vya 140/90 mmHg au zaidi, na au kama ana historia ya maumivu makali ya kichwa.