Ijumaa, 14 Aprili 2017

Tafakari ya Njia ya Msalaba Ijumaa kuu 2017.

Tafakari ya Njia ya Msalaba Ijumaa kuu 2017.



Baba Mtakatifu Francisko amemdhaminisha Professa Ann-Marie Pelletier, mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu kuandaa tafakari ya Ijumaa kuu usiku kuzunguka Magofu ya
Colosseo kwa mwaka 2017. Ni tafakari inayozingatia Vituo 14 vya Njia ya Msalaba kadiri ya Mapokeo ya Kanisa Katoliki, lakini tafakari inayogusa maisha ya familia ya Mungu kwa nyakati hizi. Professa Pelletier katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kuna baadhi ya matukio ya Njia ya Msalaba ya Yesu kuelekea mlimani Kalvari yanabeba uzito wa hali ya juu kabisa kama kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, chemchemi ya haki, amani, upendo na msamaha wa kweli.
 
Kitendo cha Mtakatifu Petro kumkana Yesu mara tatu kinaonesha udhaifu wake wa kibinadamu kwa kutojikita zaidi katika uaminifu, ujasiri na ushuhuda ambao ungekuwa na mvuto mkubwa pamoja na mashiko, lakini anaamua kuogelea katika aibu ya uwongo, hali ambayo inamkutanisha uso kwa uso na Yesu anayeteseka. Kilio cha Mtakatifu Petro kinasafisha dhamiri yake na hivyo kumwezesha kuanza safari ya kumfuasa Kristo Yesu hadi siku ile atakapofufuka kwa wafu na kumkiri kuwa ni Bwana, tayari kulinda na kuliongoza Kanisa la Kristo katika uaminifu unaojenga umoja na mshikamano na Kristo Yesu. Hii ni kwa sababu katika udhaifu wake, Mtakatifu Petro ameonjeshwa huruma, upendo na msamaha wa kweli, changamoto kwa Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake.
Professa Pelletier anasema mateso na hatimaye, kifo cha Yesu Msalabani ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaotaka kuwaokoa watu wote kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kifo cha Msalaba ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya binadamu katika ulimwengu mamboleo kutokana na vita, majanga asilia, kuporomoka kwa tunu msingi za Injili ya familia; mateso na mahangaiko ya wafungwa magerezani; ukosefu wa haki msingi za binadamu; dhuluma na nyanyaso; umaskini wa hali na kipato unaopelekea makundi makubwa ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Yote haya ni mateso na mahangaiko yanayokijaza kikombe cha mateso ya Kristo Msalabani. Leo hii kuna watoto wanadhulumiwa na kunyanyaswa utu na heshima yao; wananyimwa haki ya matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi! Ni watoto ambao wamejikuta wakiwa katika mazingira magumu na hatarishi wanaoweza kutumiwa na watu waliofilisika kiimaadili na kiutu; watu wanaomezwa na ubinafsi kwa ajili ya mafao yao binafsi. Kwa namna ya pekee, wanawake wamepewa kipaumbele cha pekee katika Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo.
Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu, Mtakatifu Catharina wa Sienna na Etty Hillesum ni kati ya wanawake wa shoka wanaotajwa kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kumfuasa Kristo Yesu kwenye Njia yake ya Msalaba. Kati ya mashuhuda wa imani wanakumbukwa pia ni Wamonaki wa Tibhirine waliowawa kikatili huko Afrika ya Kaskazini kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Professa Pelletier anasema haikuwa kazi rahisi kuandaa tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, tukio muhimu sana katika kipindi hiki cha Juma kuu, Kanisa linapoadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo kwa kutumia maneno yake ambayo yanafumbata imani ya Kanisa Katoliki inayowaambata na kuwashirikisha wote.
Professa Pelletier anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumpatia dhamana ya kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba ili kuonesha pia mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake walikuwepo wakati wa mateso ya Yesu, wakakutana naye kwenye Njia ya Msalaba, Veronika, akadiri kwa ujasiri mkuu kuupangusa uso wa Yesu! Wanawake walithubutu kusimama chini ya Msalaba na kushuhudia Yesu akiinamisha kichwa na kukata roho! Wanawake wakawa wa kwanza asubuhi na mapema kwenda Kaburini, siku ile ya kwanza ya juma! Hawa ni mashuhuda wa kweli wa Fumbo la Pasaka.
Kumbe, tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2017 inawakilisha sauti ya wanawake wanaoendelea kujisadaka usiku na mchana kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia na jamii katika ujumla wake. Tafakari hii ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutembea na kumsindikiza Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba kwa kuangalia na kuguswa na hali halisi inayowazunguka kama kielelezo cha mateso na kifo cha Yesu katika ulimwengu mamboleo, ili kutambua Saa ya Yesu! Hukumu ya mateso na hatimaye Kifo cha Yesu Msalabani ni tukio linalowagusa na kuwaambata watu wote bila ubaguzi. Yesu kwa njia ya maisha, mahubiri na miujiza yake aliweza kuwasamehe watu dhambi zao; akawaponya na magonjwa yao, akawakirimia mahitaji yao msingi pamoja na kuwarejeshea tena hadhi na utu wao kama binadamu!
Huyu ndiye ambaye watu wana mdhihaki kwa kuonesha na kushuhudia unyenyekevu wa hali ya juu kabisa kama ilivyokuwa katika Fumbo la Umwilisho, Ubatizo wake Mtoni Yordani na sasa kifo cha Msalaba! Yesu anajimimina kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti! Professa Pelletier anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari juu ya imani yao, tayari kuimwilisha katika matendo, kielelezo cha imani tendaji! Watu wametopea katika imani, wanataka kumweka Mungu mbali kabisa ya maisha na vipaumbele vyao. Huruma, upendo na unyenyekevu wa Yesu iwe ni chachu ya kuimarisha imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Kila Kituo cha Njia ya Msalaba kina ujumbe mahususi kwa kila mwamini, changamoto ni kufungua masikio na akili, ili neema ya Mungu iweze kupenya tayari kuganga na kuponya udhaifu wa binadamu! Yesu alianguka mara tatu, akasaidiwa kuubeba Msalaba na Simone wa Kirene, ambaye katika matembezi yake anakutana na Yesu Msulubiwa, mwili wake umeenea na kutapakaa kwa damu, hana nguvu tena kwani wauaji wanamvuta huku na huko kana kwamba ni jambazi wa kutupwa! Simone wa Kirene ni shuhuda wa wema, upendo na huruma; mtu anayeguswa na mahangaiko ya jirani zake! Huyu ni shuhuda wa huruma ya Mungu, changamoto kubwa ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutoa kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema! Iweni na huruma, kama Baba yenu wa mbinguni! Hii ni changamoto kwa waamini kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu, kazi inayoendelezwa na Kanisa.
Professa Ann-Marie Pelletier, mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu anasema tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2017 ni mwaliko wa kusoma alama za nyakati ili kuangalia mateso na mahangaiko ya binadamu katika ulimwengu mamboleo, tayari kuonesha mshikamano wa upendo unaoongozwa na kanuni auni; tayari kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa wale wote wanaoteseka na kukata tamaa kutokana na magumu pamoja na changamoto za maisha.
Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kupambana na utamaduni wa kifo kwa kujikita katika Injili ya uhai na matumaini, kwani baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu, Ijumaa kuu, kuna Pasaka ya Bwana, ushindi dhidi ya dhambi, mauti na kifo! Njia ya Msalaba imejikita katika tafakari na sala, mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni wachamungu wanaoshuhudia ukuu, wema, huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Mungu kwa walimwengu! Binadamu wote wanaalikwa kutembea na kushiriki na Kristo Yesu katika Njia yake ya Msalaba ili kweli watu waweze kuguswa na mateso, mahangaiko na matumaini ya jirani zao. Msalaba ni muhtasari wa hekima, huruma, upendo, msamaha na upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu! Ni alama ya ukatili wa hali ya juu kabisa ambao mwanadamu anaweza kuutenda dhidi ya jirani zake kwa njia ya vita, dhuluma na nyanyaso za kila aina. Ukatili unafumbatwa katika undani wa mwanadamu, ndiyo maana hata leo hii bado kuna watu wanateseka na kudhulumiwa sana hali inayohatarisha utu na heshima yao. Historia, maisha na utume wa Wamonaki wa Tibherine liwe ni fundisho kwa wengi!
Professa Ann-Marie Pelletier anahitimisha mahojiano maalum na Radio Vatican kwa kusema kwamba, Kituo cha XIV kinaonesha kwa namna ya pekee kabisa dhamana na mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Hawa ni wanawake wanaotaka kuandaa mwili wa Yesu kwa ajili ya maziko ya heshima kama binadamu! Jumamosi kuu ni kipindi cha kimya kikuu, muda wa tafakari ya kina baada ya mateso na kifo cha Kristo Msalabani, tayari kujiandaa kwa ajili ya kushiriki Ufufuko wa Kristo Yesu. Wanawake waliguswa sana na mateso ya Kristo, wakaimarishwa kwa imani, matumaini na mapendo, kiasi cha kusimama thabiti tayari kushuhudia Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Wanawake hawa ni tofauti kabisa na walivyokuwa wale Wafuasi wa Emmau, waliokuwa wamekata tama, kiasi cha kukosa dira na mwelekeo baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Wanawake walijiandaa kupokea ujumbe wa Ufufuko wa Kristo Yesu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.


EmoticonEmoticon