Jumatatu, 27 Machi 2017

CCM yateua Makatibu wa Mikoa 31, wa Wilaya 155. ......Yaeleza msimamo wa chama kuhusu Makond

CCM yateua Makatibu wa Mikoa 31, wa Wilaya 155. ......Yaeleza msimamo wa chama kuhusu Makonda

Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuendelea kufanya mageuzi ya uongozi, muundo na mfumo, kimefanya uteuzi wa makatibu wa mikoa 31 wakiwamo wapya 20, na wa wilaya 155 ambao uteuzi wao unaanza mara moja kuanzia jana.

Pia chama hicho kimekiri kufanya mabadiliko ya kikatiba yanayolenga maeneo matatu ambayo ni misingi ya uongozi, muundo na mfumo pamoja na utawala na utendaji kwa lengo la kukijenga zaidi chama hicho, na hakuna sehemu yoyote kwenye Katiba hiyo iliyobadilishwa inayohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alisema kati ya makatibu hao walioteuliwa wa mikoa 11 ni wale waliopandishwa hadhi kutokana na utendaji wao na 20 ni wapya kabisa.

Alisema katika orodha ya makatibu hao walioteuliwa, chama hicho kilizingatia sifa hizo ikiwemo maadili, weledi, jinsia na mpango wa kuachiana vijiti kwa kuzingatia rika.

Uteuzi wa Makatibu wa CCM Mikoa…
    Arusha- ­ Elias Mpanda
    Dar es Salaam-­ Saad Kusilawe
    Dodoma- ­ Jamila Yusuf
    Geita- ­ Adam Ngalawa
    Iringa- ­ Christopher Magala
    Kagera­- Rahel Degeleke
    Katavi­- Kajoro Vyahoroka
    Kigoma-­ Naomi Kapambala
    Kilimanjaro-­ Jonathan Mabihya
    Lindi­- Mwanamasoud Pazi
    Manyara- ­Paza Mwamlima
    Mara- ­Innocent Nanzabar
    Mbeya- ­Wilson Nkhambaku
    Morogoro-­ Kulwa Milonge
    Mtwara- ­Zacharia Mwansasu
    Mwanza-­ Raymond Mwangala
    Njombe-­ Hossea Mpagike
    Pwani-­ Anastanzia Amasi
    Rukwa-­ Loth Ole Nesere
    Ruvuma­- Amina Imbo
    Shinyanga- ­Haula Kachambwa
    Simiyu-­ Donald Etamya
    Singida-­ Jimson Mhagama
    Tabora-­ Janeth Kayanda
    Tanga-­ Allan Kingazi.
“Makatibu wengi (20) tuliowateua ni wapya, hatuwezi kufanya mageuzi ya kuwa na CCM mpya na upya huo usionekane. Mageuzi ni fikra” amesema Polepole.

Lakini pia alisema katika orodha hiyo ya makatibu wa wilaya wa CCM 155, makatibu 76 ni wapya kutokana na vigezo vipya vilivyowekwa na chama hicho.

Aliwataja baadhi yao kuwa ni Mussa Matoroka anayekwenda Arumeru, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba ‘Gaddafi’ (Longido), Joyce Mwenda (Namtumbo), Kombo Kamote (Bagamoyo), Grevas Ndaki (Momba), Othman Dunga (Hanang), Pili Augustino (Dodoma Mjini) na Martin Mwakitabu (Chamwino).

Wengine ni Aveline Ngwada (Bukombe), Nuru Ngeleja (Chato), Michael Mbaga (Iringa Mjini), Afidu Luambano (Temeke), Joyce Mkaugala (Ilala), Hanaf Msabaha (Kinondoni), Salum Kali (Ubungo), Robert Kalenge (Kigamboni), Ramadhan Dallo (Arusha) na Gulisha Mvanga (Monduli).

Kuhusu suala la Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Polepole alisema, kwanza napenda kusema kuwa uhusiano wa CCM na vyombo vya habari ni wa kihistoria’… CCM inapenda kufuata utaratibu na ndio salama yetu kama yupo kiongozi wa chama amefanya jambo tuna utaratibu mzuri wa kuchunguza. Lakini pili, Mkuu wa Mkoa ni mteule wa Rais na anapomteua anamteua yeye peke yake na halazimiki kushauriana na mtu, hivyo badala ya kukaa na kumpangia Rais kitu cha kufanya, tumuache afanye kazi’.. “

Aidha, Humphrey Polepole akitolea ufafanuzi madai yanayoenezwa kuwa wamefanya mabadiliko kuwa Rais Magufuli ndiye atakayegombea 2020 bila kupingwa amesema kuwa, mabadiliko ya katiba waliyoyafanya katika mkutano mkuu maalum, hayakuhusu mchakato wa kumpata mgombea wa uchaguzi mwaka 2020. Hivyo tunawaomba wanachama wetu na watanzania wapuuze habari nyingine zinazoenezwa.

Katibu wa CCM itikadi na Uenezi ­Taifa